Barkley pigo kwa Everton

Everton wamepata pigo kubwa, kutokana na kuumia kwa kiungo wao chipukizi na mahiri, Ross Barkley.
Kocha Roberto Martinez amesema kwamba Barkley (20) anaweza kuwa nje ya dimba kwa hadi miezi mitano, kutokana na kuumia goti wakati akiwa kwenye mazoezi Ijumaa hii.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alichunguzwa juu ya kuumia kwake lakini hawakuweza kubaini mapema kutokana na uvimbe mkubwa, na sasa Martinez anasema anaweza kuwa nje kuanzia wiki saba hadi miezi mitano.

Iwapo atakuwa nje kwa muda mrefu atakosa pia mechi za England za kufuzu kwa michuano ya Euro 2016 dhidi ya San Marino na Estonia zilizopangwa kuchezwa Oktoba mwaka huu. Barkley alicheza mechi 34 Everton msimu uliopita wa ligi kuu na kufunga mabao sita.

Mchezaji huyo nyota alikuwa kwenye kikosi cha England kilichoshiriki na kutolewa mapema kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka huu, akianza kucheza akitokea benchi kwenye mechi dhidi ya Italia ambapo England walilala 1-2. Alianza kuchezea klabu hiyo msimu wa 2011/12.

Kinda huyo alicheza mechi zote tatu za kabla ya msimu baada ya kurudi kutoka Brazil na alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha Martinez, na sasa alikuwa akijiwinda kuwa katika kikosi cha kwanza cha England chini ya Roy Hodgson.

Aliumizwa na mchezaji mwenzake wakati wa mazoezi kwa bahati mbaya, lakini Martinez anadai kwamba kikosi chake ni kikubwa hivyo kwamba hapatakiwi kuwapo pengo, japokuwa watamkosa Barkley. Katika mechi ya kwanza msimu huu wa ligi, Everton walikwenda sare ya 2-2 na Leicester.

Comments