Barcelona watangaza manahodha wanne

Vigogo wa soka wa Hispania, Barcelona wametangaza majina manne ya manahodha wao kwa msimu wa 2014/15, kutokana na nahodha wake, Carles Puyol na msaidizi, Victor Valdes kuhama.

Barca ambao msimu uliopita hawakuambulia kombe lolote, na wapo chini ya kocha mpya, Luis Enrique, wataogozwa na  Xavi Hernandez kama nahodha namba moja huku Andres Iniesta akishika namba mbili.

Xavi alikuwa nahodha msaidizi kwa miaka sita hapo Camp Nou wakati Iniesta alikuwa namba tatu. Wapya waliochaguliwa na kikosi cha Barca kuwa manahodha namba tatu na nne ni  Lionel Messi naSergio Busquets.

Puyol aliyechezea Barcelona tu katika maisha yake ya soka, alitangaza kustaafu soka kiangazi hiki, kutokana na kuumia mara kwa mara kiasi kwamba alisema hataweza kuhimili mikiki ya ligi kubwa ya Hispania, lakini alikuwa na mawazo kwamba akishapumzika anaweza kupata timu nyingine.

Valdes alimaliza mkataba wake na hakupenda kusaini mwingine, lakini akapata pigo kubwa baada ya kuumia na kulazimika kuwa nje kwa muda mrefu. Alitarajia kujiunga na Monaco lakini bado mambo hayajatengamaa.

Comments