Celtic warejeshwa Ligi ya Mabingwa

Klabu Bingwa ya Uskochi, Celtic wamerejeshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kutokana na wapinzani wao, Legia Warsaw kuchezesha mchezaji asiye na sifa.

Celtic walikuwa wametolewa na timu hiyo na Wapolishi hao ambao waliwasasambua kwa wastani wa mabao 6-1 katika awamu ya tatu ya kutafuta watakaofuzu kwa UCL msimu ujao.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) limeamua kuwatupa nje  Legia kutokana na kumchezesha Bartosz Bereszynski kwenye mechi ya mkondo wa pili wakati alikuwa na kadi nyekundu.

Kwa maana hiyo, Celtic wamepewa ushindi wa mabao 3-0 na kusonga mbele kwenye mchakato huo, tena yakiwa ni mabao ya ugenini. Baadaye mwezi huu, Celtic watacheza na Maribor kutoka Slovenia. Hata hivyo, Legia wamepewa siku tano kukatia rufaa uamuzi huo wakipenda.

Mabingwa hao wa Poland sasa wametupwa kucheza mechi za kufuzu kwa ajili ya Ligi ya Europa. Walikuwa wamewashinda Celtic 4-1 kwenye mechi ya kwanza kisha wakawakandamiza 2-0 kwenye marudiano.

Kocha wa Celtic, Ronny Deila alikuwa amesema kwamba licha ya kutolewa timu yake ilifanya vyema na kuahidi kuendelea nayo vizuri zaidi katika mashindano mengine. Deila alichukua mikoba ya Neil Lennon aliyeamua kujiuzulu licha ya kuwapa ubingwa wa Uskochi msimu uliopita.

Bereszynski
Bereszynski

Kamati ya Nidhamu ya Uefa imesema kwamba Bereszynski amepigwa marufuku kucheza mechi moja zaidi. Alipata kadi nyekundu kwenye mechi msimu uliopita dhidi ya Apollon Limassol na kuzuiwa kucheza kwa mechi tatu.

Ofisa wa Legia, Dominik Ebebenge amedai kwamba haki haikutendeka na adhabu waliyopewa si sahihi, akidai suala kama hilo lilipata kutokea siku zilizopita lakini adhabu haikufanana na waliyopewa, akidai ni kosa la kibinadamu tu.

Ebebenge amesema wamefanyia kazi kwa miaka minane ili kufuzu kucheza UCL, wameshinda vyema mechi zao mbili lakini wanapokonywa tonge mdomoni hivi hivi. Celtic walipata kufanya kosa kama hilo lakini Uefa wakawapa onyo tu.
Makosa kama hayo yamekuwa ya kawaida kwa mataifa ya Afrika kwenye mashindano mbalimbali, ambapo timu zimepata kupewa adhabu ya kutupwa nje ya michuano.

Comments