Arsenal kuwakabili Besiktas

Arsenal wamepangwa kucheza na Besiktas katika mechi mbili zitakazoamua nani asonge mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Vijana hao wa Arsene Wenger wanatafuta kuvuka hatua hiyo kwa mara ya 15 mfululizo. Wanalazimika kucheza mechi ya kufuzu kwa vile walimaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliopita.

England huwakilishwa na timu nne kwenye mashindano hayo, na hiyo ni kulingana na ubora wa timu katika ligi ya nchi husika. Klabu zilizofuzu kwa hatua ya makundi kutoka England ni Manchester City, Liverpool na Chelsea.

Besiktas walimaliza katika nafasi ya tatu nchini Uturuki na wanafundishwa na beki wa zamani wa West Ham na Everton, Slaven Bilic, ambapo kikosi chao kinaye mshambuliaji Demba Ba aliyeuzwa huko kutoka Chelsea kiangazi hiki.

Ba aliyeuzwa kwa pauni milioni 4.7ndiye aliwapatia Besiktas bao la ushindi kwenye raundi iliyopita ya mchujo. Huu ni msimu wa pili mfululizo wanapangwa na wapinzani kutoka Istanbul, kwani msimu uliopita walicheza na Fenerbahce na kuwatoa kwa jumla ya mabao 5-0 katika mechi zao mbili.

Mechi za kwanza katika mchujo huu zitafanyika Agosti 19 au 20 na marudiano ni wiki moja baadaye na mshindi ataingia kwenye hatua za makundi.

Ratiba iliyotoka inaonesha kuwa Maribor (Slovenia) watacheza na Celtic (Scotland), Salzburg (Austria) watakabiliana na Malmo (Sweden), Aalborg (Denmark) watakwaana na Apoel Nicosia (Cyprus) wakati Steaua Bucharest (Romania) watajipima na Ludogorets (Bulgaria).

Mechi nyingine ni Slovan Bratislava (Slovakia) dhidi ya BATE Borisov (Belarus), Standard Liege (Ubelgiji) na Zenit St Petersburg (Urusi), FC Copenhagen (Denmark) na Bayer Leverkusen (Ujerumani), Lille (Ufaransa) dhidi ya Porto (Ureno)na Napoli  ya Italia wakicheza na Athletic Bilbao kutoka Hispania.

Comments