Howard Webb astaafu urefa

Mwamuzi wa soka, Howard Webb aliyejipatia umaarufu mkubwa duniani kwa ujumla amestaafu rasmi kazi hiyo.

Webb (43) ameachia ngazi baada ya kuwa mwamuzi kwa miaka 25 na sasa atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Waamuzi, baada ya kuwa amesimamia jumla ya mechi 500.

Alimaliza kazi yake kwa kuchezesha mechi za fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka huu. Alianza kazi hiyo 1989 katika mikoa ya kaskazini ya England kabla ya kupanda ngazi 2003.

Webb anayejulikana pia kwa utata kwenye baadhi ya maamuzi yake, hasa kuhusiana na klabu ya Manchester United ambayo baadhi wanadai alikuwa akiibeba na kuna habari kwamba ni shabiki wa klabu hiyo, japokuwa kuna maamuzi mengine aliwang’ata.

image
Amesema anasubiri kwa hamu kuanza ukurasa mpya katika maisha yake, baada ya kuwa amechezesha mechi katika mashindano tisa makubwa ya kimataifa, ukiachilia mbali Ligi Kuu ya England (EPL) ambamo alikuwa akipuliza kipenga kwenye mechi nyingi kubwa.

Ndiye alichezesha mechi ya makundi baina ya Colombia na Ivory Coast na ile ya kwanza ya mtoano baina ya Brazil na Chile. Mwaka 2011 Webb alitunukiwa tuzo ya heshima ya Falme ya Uingereza.

Majukumu mapya ya Webb yatakuwa kusimamia maelekezo ya kiufundi kuhusiana na waamuzi wa soka na amesema huo ni mwanya wa kuandaa waamuzi wapya watakaokuwa wazuri kwenye soka Uingereza na duniani kwa ujumla.

Webb alizaliwa Rotherham, Yorkshire na baba yake, Billy Webb alikuwa mwamuzi kwa muda wa miaka 35.

Comments