Bondia Kidunda hoi Madola

Bondia aliyekuwa tegemeo kwa Tanzania katika michuano ya Jumuiya ya Madola inayoendelea Glasgow, Uskochi, Selemani Kidunda amepigwa.

Kidunda ambaye ndiye nahodha wa Timu ya Madola ya Tanzania alipoteza pambano lake dhidi ya Mnigeria Kehinde Ademuyiwa kwa pointi katika pambano la uzito wa kilo 69.

Hata hivyo, Kidunda alijitahidi na kupoteza kwa uchache wa pointi, kwani alinyakua 28 dhidi ya 29 za Mnigeria kutoka kwa majaji watatu.

Ademuyiwa sasa anasonga mbele kwenye hatua ya 16 na atachuana na bondia wa Australia, huku Mtanzania mwingine, Nasser Mafuru akipoteza kwa raia wa Ghana, Jessie Lartey katika ndondi za uzani wa kilo 60.

Mtanzania mwingine, Fabian Gaudence  alitarajiwa kukabiliana na Mmalawi Steven Tanki usiku wa kuamkia leo na Joseph Martin alikuwa achuane na Mnamibia Mudandjae Kasuto kwenye uzani wa kati wa kilo 75.

Katika tukio jingine, mwanariadha maarufu wa Jamaica, Usain Bolt amevuta hisia za watu baada ya kuwasili nchini Uskochi tayari kuonesha vitu vyake katika mashindano yanayoonekana kususiwa na wachezaji kadhaa mashuhuri.

Comments