Drogba arudi Chelsea

Mshambuliaji mkongwe wa Ivory Coast, Didier Drigba amesaini mkataba wa mwaka mmoja katika klabu yake ya zamani ya Chelsea.

Drogba aliyeondoka hapo na kwenda kucheza Galatasaray amerejeshwa na Jose Mourinho aliyesema kwamba Stamford Bridge ni nyumbani kwa Drogba na amemsajili bila ada ya uhamisho kwani mkataba wake Uturuki ulishamalizika.

Drogba (36) alizoa makombe 10 akiwa Chelsea alikohudumu tangu 2004 hadi 2012 na amesema ilikuwa rahisi sana kufanya uamuzi huo, kwani baada ya Chelsea kumpa ofa hangeweza kukataa kufanya kazi na Mourinho anayemhusudu.

Amesema anasubiri kwa hamu kuonesha mikogo yake katika soka kwenye msimu mpya unaoanza mwezi ujao ili kuisaidia timu hiyo kufanya vyema. Msimu uliopita Chelsea hawakuambulia taji hata moja.

Drogba alijiunga Chelsea akitokea Marseille ya Ufaransa kwa kitita cha pauni milioni 24 na aliondoka baada ya kuifungia timu bao la ushindi katika mikwaju ya penati dhidi ya Bayern Munich kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini mkataba wake haukuongezwa.

Baada ya hapo alijiunga na klabu ya Uchina ya  Shanghai Shenhua, kabla ya kuondoka kwa utata kwenda Uturuki na Galatasaray wakatwaa ubingwa wan chi hiyo ambapo yeye alifunga mabao 10 katika mechi 32.

Comments