Van Gaal aanza ngebe

Kocha Mkuu wa Manchester United, Louis van Gaal ameuchana mpangilio wa ziara ya kabla ya msimu wa timu hiyo nchini Marekani.

Mdachi huyo amesema kwamba wanachofanya ni kama matangazo ya biashara ambapo wanalazimika kusafiri mara nyingi katika muda mfupi, akisema si jambo jema kwa timu inayoajiandaa na ligi kuu ngumu.

“Yaani mnasafiri umbali mrefu kweli, mnatumia ndege sana kuruka hivyo kwamba mnakuwa na uchovu wa safari. Hiki si kitu kizuri kama kweli tunafanya maandalizi,” akasema Van Gaal ambaye pia ameshangazwa na uwanja wa mazoezi wa Carrington ambao una sehemu upepo unavuma sana na tayari ameagiza marekebisho.

United wanaanza mechi zao Jumatano hii Pasadena, kabla ya kwenda Denver, Washington na Detroit. Van Gaal, hata hivyo, alisema kwa kuwa ziara ilipangwa na kuidhinishwa akiwa hajaanza kazi, hataibadilisha.

 Kauli yake hiyo inapingana na ya Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward aliyotoa saa 24 kabla, akisisitiza kwamba ziara hiyo haiwezi, kwa namna yoyote ile kuvuruga maandalizi. United wanatarajiwa kusafiri jumla ya umbali wa maili  13,500.

Hata hivyo, Van Gaal amesema lazima Man U lazima wafuate kanuni zake ili maandalizi hayo yaende vizuri. Siku ya kwana kukanyaga United, Van Gaal alisema kwamba yeye ni mwanademokrasia, akawachagiza waandishi waliodai kuwa ni mkali sana.

Amesema kwamba mwaka ujao watafanya ziara fupi na katika eneo moja, akisema ana uhakika wa kulitekeleza hilo. Man United wamenunuliwa na Familia ya Glazer, hivyo siku hizi ziara zao za kabla ya msimu hufanyika nchini Marekani.

Comments