Rais Argentina hapendi soka

*Awakata maini kina Messi, Sabella

Rais wa Argentina, Cristina Fernandez de Kirchner amekipokea kikosi cha Argentina kilichokosa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa kufungwa 1-0 na kukiongezea simanzi na upweke.

Mwanamama huyo aliwahutubia kinyonge, wakati mwingine akitabasamu lakini alishindwa kuchagua maneno yake hivyo kwamba wachezaji walijiona kana kwamba wapo kwenye kitu kisicho na maana.

Rais Kirchner alimpa nafasi Lionel Messi kuzungumza, nahodha huyo akasema wangependa kurejea na kombe kama yalivyokuwa matarajio ya wananchi, walijitahidi sana lakini jitihada zao hazikutosha.

Ilipofika zamu yake, badala ya rais kuwafariji, aliwapa pigo kubwa la kikatili kwa kusema kwamba hakutazama hata mechi moja tangu walipoanza kwenda huko, wachezaji wakabaki kumwangalia kwa mshangao.
“Kama mjuavyo, mie si shabiki wa soka. Sikutazama hata mechi moja, wala ile ya Jumapili sikuitazama,” akasema akiwa amesimama na Messi na kocha Alejandro Sabella. ”

Ilikuwa imetangazwa mapema kwamba Rais Kirchner aliyepewa mwaliko rasmi na Rais Dilma Rouseff wa Brazil kuhudhuria hafla na fainali hiyo, hangekwenda nchi jirani kabisa ya Brazil, kwa madai kwamba alikuwa anahisi koo lina uchachu.

Lakini Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliyepata mwaliko sawa na wake alifunga safari ndefu ya kuvuka bahari, mabonde na milima hadi Rio de Janeiro. Mbaya zaidi ni kwamba marais wote watatu – mwenyeji na wa timu zilizokuwa zikicheza fainali ni wanawake.

Rais Vladimir Putin pia alifunga safari kutoka kwao hadi hapo, akiwa mmoja wa wageni maarufu. Urusi wanaandaa michuano ijayo ya Kombe la Dunia 2018

Comments