Fifa yataja wanaowania tuzo

Wachezaji wanaowania tuzo katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu wametajwa, ambapo Ujerumani wametoa wane huku Argentina wanaochuana nao Jumapili hii katika fainali wakitoa watatu.

Wachezaji waliochaguliwa kutoka timu ya Ujerumani inayofundishwa na Joachim Low kuwania mchezaji bora ni Mats Hummels, Toni Kroos, Phillip Lahm na Thomas Muller.

Kwa upande wa Argentina, waliochujwa ni Angel Di Maria, Javier Mascherano na Lionel Messi.

Katika orodha ya wachezaji 10 watakaopambanishwa, wapo pia James Rodriguez wa Colombia,  Neymar wa Brazil na Arjen Robben wa Uholanzi.

Wanaowania nafasi ya kipa bora wa mashindano haya ni watatu; yule wa Costa Rica, Keylor Navas; wa Ujerumani, Manuel Neuer na wa Argentina, Sergio Romero.

Wakati huo huo, wachezaji walioteuliwa kwa ajili ya kuwania tuzo ya mchezaji bora mwenye umri mdogo ni Memphis Depay wa Uholanzi, Paul Pogba na Raphael Varane wa Ufaransa.

Washindi wa tuzo zote hizo watatangazwa baada ya mechi ya fainali Jumapili hii baina ya Argentina na Ujerumani.

Comments