Simba kuanza mazoezi leo

KIKOSI cha Simba ya jijini Dar es Salaam kinatarajia kuanza mazoezi leo kwenye Uwanja wa Boko Veteran ulioko Boko kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara imeelezwa.

Akizungumza nami jana, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa tayari wachezaji wa timu hiyo wameshapewa taarifa za kuanza kwa mazoezi hayo tayari kunoa makali kwa msimu mpya wa ligi.

Kamwaga alisema kuwa licha ya kuchelewa kuanza maandalizi yake, wanaamini wachezaji watakuwa kwenye kiwango cha juu kutokana na kila mmoja kufanya mazoezi binafsi.

“Kabla mwalimu ( Zdravko Logarusic) hajaondoka, aliwaeleza wachezaji wajitunze na wawe wanafanya mazoezi ili kujiweka tayari na programu alizoziandaa za msimu mpya,” alisema kiongozi huyo.

Kikosi hiko kinatarajia kuanza mazoezi chini ya kocha msaidizi, Selemani Matola, kutokana na Logarusic, kuchelewa kuwasili nchini kama ilivyotarajiwa.

Habari za ndani zilizopatikana jana mchana zinasema kwamba Mcroatia huyo atawasili nchini Alhamisi na Ijumaa ataungana na wachezaji wake kuendelea na mazoezi.

Simba pia inatarajia kuelekea Afrika Kusini kuweka kambi ya siku 17 na itaondoka nchini Julai 20.
Hata hivyo katika kambi hiyo huenda ikawakosa nyota wake watano walioko katika timu ya Taifa (Taifa Stars) ambao wanajiandaa kuikabili Msumbiji.

Nyota hao ni pamoja na Ramadhan Singano ‘Messi’, Amri Kiemba, Jonas Mkude, Joram Mgeveke na Haroun Chanongo.

Comments