Wastaafu wa Real Madrid kuzuru Tanzania

Maandalizi ya kuwaleta wachezaji wakongwe wa timu ya Real Madrid kutoka Hispania yamekamilika, imeelezwa jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo jijini, Afisa Uhusiano wa kimataifa wa Real Madrid, Rayco Garcia, alisema kuwa tayari nyota tisa waliowahi kutamba na timu hiyo kongwe wamethibitisha kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu.
Garcia aliwataja nyota hao kuwa ni pamoja na Michael Owen, Luis Figo, Michell Salgado, Cannavaro, Christian Karembeu, Fernando Orientes, Steve Maccmanaman, Reuben De la Red na Fernando Huierro.

Alisema kuwa ziara ya timu hiyo inatarajia kuwa na watu 50, ambao ni wachezaji pamoja na familia zao.
Alieleza kuwa pia wanatarajia kuongozwa na Waziri wa Utalii wa nchi hiyo ambaye naye amevutiwa kuja Tanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

” Hii ni nafasi kubwa kwa nyota hao kutembelea Afrika na huu ni mwanzo mzuri wa kuwezesha kikosi cha Real Madrid cha sasa kuja Tanzania,” alisema mwakilishi huyo wa Tanzania .

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya TSN Group ambao wanadhamini ziara ya timu hiyo, Dennis Ssebo, alisema kuwa maandalizi yako katika hatua za mwisho na wanaamini ujio huo utalisaidia taifa kujiongezea kipato.

Ssebo alisema kuwa wakongwe hao watatua nchini Agosti 22 na mechi yao itafanyika siku inayofuata kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Aliongeza kuwa baada ya mechi hiyo dhidi ya nyota mbalimbali waliowahi kutamba Tanzania, wataelekea Arusha kwa ajili ya kushiriki tukio kubwa litakalotangazwa hapo baadaye.

Ujio huo ni sehemu ya kutangaza vivutio vya utalii vyahapa nchini ikiwamo mbuga ya wanyama ya Serengeti.

Comments