Ubelgiji, Argentina robo fainali

Ubelgiji na Argentina wamekata tiketi ya kuingia robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia.

Wakati Ubelgiji waliwafunga Marekani 2-1, Argentina walitokwa jasho kuwashinda Uswisi 1-0, mechi zote zikienda hadi muda wa nyongeza.

Kizazi cha dhahabu cha Ubelgiji kilichanua ikiwa ni mara ya kwanza katika miaka 28 kufika hatua hiyo. Mabao ya Ubelgiji yalifungwa na Kevin de Bruyne na Romelu Lukaku.
Ubelgiji walimwanzisha kinda wao kutoka Kenya, Divoc Origi aliyebadilishwa na Lukaku dakika ya 90 na Origi alikaribia kufunga mara kadhaa. Marekani walipata bao kupitia kwa Julian Green.

Argentina walipata ushindi kwa shida baada ya kubanwa muda mrefu na Uswisi, ambapo Angel Di Maria ndiye alifunga bao pekee la mechi hiyo.

Mabingwa hao wa mara mbili walitawala mchezo lakini ilikuwa vigumu kufanikiwa kucheka na nyavu licha ya kuwa na Lionel Messi.

Argentina sasa watakabiliana na Ubelgiji katika robo fainali Jumamosi hii. Di Maria, hata hivyo, alipoteza nafasi nyingi za kufunga lakini hakukata tamaa.

Argentina waliungwa mkono na washabiki kadiri ya 40,000 kwenye dimba la Arena de Sao Paulo ambapo bao la Di Maria liliwafanya washangilie kwa nguvu kubwa.

Comments