Kocha, nahodha Nigeria wajiuzulu

Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi na nahodha Joseph Yobo wamejiuzulu baada ya timu yao kutolewa na Ufaransa kwenye hatua ya 16 bora ya Fainali za Kombe la Dunia.

Super Eagles walifungwa 2-0 Jumatatu hii, ambapo Wafaransa walifunga mabao yote katika dakika 11 za mwisho.

Keshi (52) aliteuliwa katika nafasi hiyo 2011 na aliwawezesha Nigeria kutwaa ubingwa wa Afrika miaka miwili baadaye.

Nahodha Yobo (33) amesema ni wakati wa chipukizi kuchukua jahazi, lakini akiamini kwamba timu ina mwelekeo mzuri na itapata mafanikio makubwa.

Mchezaji huyo wa Fenerbahce alijifunga bao dakika za mwisho wa mchezo baada ya Paul Pogbawa Ufaransa kufunga bao la kwanza, akimaliza ubishi wa beki ya Nigeria.
20140701-121540-44140837.jpg

Keshi alitoa barua ya kujiuzulu mwaka jana baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika, akisema sababu ni kutoheshimiwa wala kuungwa mkono lakini alishawishiwa na waziri wa michezo na akakubali kubaki.

Nigeria waliwashinda Bosnia-Hercegovina katika hatua ya makundi baada ya kwenda suluhu na Iran kisha wakafungwa na Argentina kwa tabu.

Hii ni mara ya kwanza kwa Nigeria kuvuka hatua ya makundi tangu 1998 licha ya wachezaji kuhusika katika mgomo juu ya posho.

Yobo amechezea Super Eagles mechi 100 na kuvunja rekodi ya Jay-Jay Okocha kucheza mechi za Kombe la Dunia kwa mechi tisa.

Keshi anakuwa kocha wa sita kuachia ngazi wakati wa fainali hizi za Kombe la Dunia.

Wengine walioachia ngazi ni kocha wa Honduras, Luis Suarez; wa Iran, Carlos Queiroz; wa Japan, Alberto Zaccheroni; wa Italia, Cesare Prandelli na yule wa Ivory Coast, Sabri Lamouchi.

Keshi alikuwa nahodha wa Nigeria mwaka 1994 kwenye fainali za Kombe la Dunia na kabla ya kuwafundisha Super Eagles alikuwa kocha wa Mali na Togo.

Yobo amecheza mechi za Kombe la Dunia katika fainali za mwaka 2002, 2010 na 2014.

Comments