Nigeria wafungishwa virago

*Algeria watolewa kwa taabu na Ujerumani
Timu ya Taifa ya Nigeria imefuata nyayo za wenzao waliopata kugoma kwa kufungishwa virago na Ufaransa.
Mabingwa hao wa Afrika waliingia katika mtego mbaya wa kutaka posho ili wajishughulishe vilivyo na majukumu yao na rais wa nchi aliingilia kati.
Licha ya kuahidiwa kwamba wangelipwa fedha zao, Nigeria kama walivyokuwa Ghana na nyuma yao Cameroon, walitolewa kwenye mashindano.
Mabao yalifungwa na Paul Pogba katika dakika ya 79 ambaye saini yake inawindwa na timu kadhaa katika ligi maarufu duniani wakati nahodha wa Nigeria, Joseph Yobo alijifunga dakika ya 90.
Katika hali hii, Nigeria walijitahidi kuzuiwa kutofungwa kwa muda mrefu, lakini tatizo ni kwamba hawakutafuta au hawakupata bao au mabao.
Ilivyokuwa ni kwamba Ufaransa walipata mabao yao ndani ya dakika 11 za mwisho jijini Brasilia na kupeleka majonzi kwa mabingwa hao wa Afrika, lakini pia kwa Afrika kwa ujumla.
Nigeria walifanikiwa kutikisa nyavu kupitia kwa
Emmanuel Emenike lakini bao likakataliwa kwa maelezo kwamba alikuwa ameotea. Ilikuwa muda mfupi tu kabla ya kipa wa Nigeria, Vincent Enyeama kumkatalia Pogba kutikisa nyavu zake kwa mpira wa juu.
Hata hivyo Pogba alifunga baadaye, huku mchezaji wa Liverpool, Victor Moses akiokoa mpira wa Karim Benzema katika mstari wa goli.
Mabingwa hao wa Afrika walilazimika kubadili wachezaji, baada ya kiungo wao muhimu, Ogenyi Onazi kuumizwa na Blaise Matuidi ambaye alikuwa na bahati ya kutopewa kadi.

Comments