Waziri wa michezo Ghana nje

 

SIKU moja baada ya Ghana kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia, waziri wa michezo na naibu wake wameondolewa wizarani.

Rais John Mahama amechukua hatua hiyo baada ya Ghana kumaliza wa mwisho kwenye kundi lao huku rais mwenyewe akiagiza wachezaji wapelekewe posho zao kabla ya kuwakabili Ureno.

Wachezaji waligoma baada ya kutolipwa posho ya ushiriki wa fainali hizo, ambapo walianza kwa kufungwa na Marekani, wakaenda sare na Ujerumani kabla ya kufungwa na Ureno.

Walikuwa na nafasi ya kusonga mbele, lakini mgogoro wa posho uliwachepua na kisha wachezaji wawili muhimu, Kevin-Prince Boateng na Sulley Muntari walifukuzwa kambini saa chache kabla ya mechi dhidi ya Ureno.

Pamoja na kuwa kwenye kundi gumu, Ghana walioesha uwezo mkubwa dhidi ya Ujerumani.
Taarifa ya Rais Mahama ilisema kwamba Waziri wa Michezo, Elvis Afriyie-Ankrah anakuwa Waziri wa Nchi na aliyekuwa naibu wake, Joseph Yammin anapelekwa kuwa Waziri wa Jimbo la Ashanti.

Rais aliingilia kati na kutoa posho zilizopelekwa Brazil pauni milioni 1.8 taslimu kwa wachezaji kwa kutumia ndege ya kukodi.

Boateng (27) anayechezea Schalke 04 ya Ujerumani alifukuzwa kwa madai ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya kocha Kwesi Appiah wakiwa mazoezini.

Muntari (29) anayekipiga AC Milan ya Italia, alimpiga mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FA, Moses Armah.

Ili kufuzu, Ghana walitakiwa kushinda mechi dhidi ya Ureno na kuomba apatikane mshini baina ya Marekani na Ujerumani, ambapo Ujerumani walishinda.

Comments