Lalana kumbadili Suarez Liverpool

 

Baada ya Luis Suarez kufungiwa kwa miezi minne, klabu yake ya Liverpool inakamilisha usajili wa Adam Lalana kwa paui milioni 25.

Suarez aliyefungiwa na Fifa kwa kumng’ata Giorgio Chiellini wa Italia ndiye alikuwa mfungaji bora wa Liverpool misimu miwili iliyopita na bora kwa England msimu ulimalizika.

Kufungiwa kwake kunamaanisha Liverpool watamkosa kwa mechi karibu 10 za mwanzo msimu ujao, lakini walikuwa wanakamilisha usajili wa mpachika mabao wa Southampton, Lalana.

Klabu mbili hizo zilikubaliana ada Ijumaa hii na Lalana (26) anakamilisha vipimo vya afya na mambo mengine wikiendi hii ili ahamishie majeshi Anfield kutoka St Mary’s mapema wiki ijayo.

Lalana amekuwa akicheza Southampton kwa miaka 14, kwani alijiunga hapo akiwa na umri wa miaka 12. Ofa ya kwanza ya mchezaji huyo wa Timu ya Taifa ya England ilikataliwa na Saints lakini baada ya kutoka kwenye fainali za Kombe la Dunia, Liverpool waliipeleka tena mezani, ikakubaliwa.

Southampton wanaendelea kuodokewa na wachezaji wake mahiri, kwani beki wa kushoto, Luke Shaw amesajiliwa na Manchester United huku Liverpool wakitangulia kumsajili Rickie Lambert.

Liverpool wanaonekana kukiri kwamba hawataweza kufikia kiwango cha juu cha soka kama msimu uliomalizika iwapo hawatajiimarisha, maana pia hawajui hatima ya Suarez.

Barcelona wanadaiwa kutaka kumsajili mshambuliaji huyo wa Uruguay licha ya kutiwa hatiani kwa mara ya tatu kwa kung’ata wachezaji wa timu pinzani dimbani.

Kocha Brendan Rodgers anadaiwa kuwa katika mipango ya kumsajili mshambuliaji wa Benfica,
Lazar Markovic na mshambuliaji kinda wa Ubelgiji mwenye asili ya Kenya, Divock Origi.

Siku ya kwanza ya msimu wa Ligi Kuu England itakuwa ya hisia za aina yake kwa Southampton kwani watakuwa wageni wa Liverpool waliowapokonya wachezaji wao wawili.

Kuna habari kwamba shabiki mmoja wa Saints amemvaa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger nchini Brazil kumsihi kutomsajili Morgan Schneiderlin kutoka St Mary’s, kwani ngome yao inabomoka.

Wenger nayedaiwa kumhusudu na kuwa na mpango wa kumsajili mchezaji huyo wa kiungo aliishia kucheka tu.

Lalana atatakiwa kujenga upili na Daniel Sturridge ambaye msimu uliopita alishirikiana vyema na Suarez kutesa ngome za timu pinzani na kuibuka wafungaji wazuri zaidi kundini.

 

 

Comments