‘Suarez anahitaji tiba’

 

*Barcelona bado wataka kumsajili

 

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Jerome Valcke amesema anaamini Luis Suarez ana matatizo na anahitaji tiba.

 

Valcke anasema hayo siku moja baada ya shirikisho lake kumpa adhabu kubwa ya kukosa mechi tisa za kimataifa na kutojishughulisha na masuala ya soka kwa miezi minne pamoja na faini kubwa.

 

Tatizo la Suarez ambalo ametiwa nalo hatiani kwa mara ya tatu na taasisi tatu tofauti ni kung’ata wanasoka wa timu pinzani, shingoni, mkononi na begani.

 

Katibu mkuu wa Fifa amesema kwamba sasa Suarez, mshambuliaji wa Uruguay aliyeadhibiwa Alhamisi hii kwa kumng’ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini anatakiwa kwenda kutafuta matibabu.

 

Mkongwe wa soka, Diego Maradona naye amesema baada ya tukio hilo na adhabu sasa jitihada zinatakiwa zielekezwe kumtafutia tiba.

 

Hata hivyo, Valke anaunga mkono adhabu aliyopewa, akisema inatakiwa kuwa mfano ili mhusika ajifunze na wengine wasirudie kitendo kama hicho. Suarez pia amepigwa faini ya pauni 65,680.

 

Licha ya madhila yote yaliyomkumba Suarez na kufungiwa kwake hadi mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, klabu ya Barcelona wamesema kwamba bado wanamhitaji mchezaji huyo.

 

Wanasema hivyo wakati Liverpool anayochezea wakitafuta ushauri wa kisheria juu ya lipi la kufanya kuhusu uamuzi wa Fifa na juu ya mchezaji wao huyo ambaye ameongoza kwa kpachika mabao msimu uliomalizika.

Comments