Algeria wavuka, Ghana nje

Algeria wamefanikiwa kuvuka hatua ya makundi, baada ya kwenda sare ya 1-1 na Urusi kwenye mechi ya mwisho ya makundi.

Kocha Vahid Halilhodzic anasema bado hawajasahau sintofahamu iliyotokea 1982 walipokutana na Ujerumani, ambao wanajiandaa tena kukutana nao kwenye hatua ya mtoano katika 16 bora.

Algeria walishiriki fainali hizi kwa mara ya kwanza nchini Hispania mwaka huo ambapo waliwafunga Ujerumani Magharibi 2-1, wakati huo Ujerumani wakiwa ndio mabingwa wa Ulaya.

Katika mechi nyingine, wawakilishi wa Afrika, Ghana walishindwa kutumia faida ya Ujerumani kuwafunga Marekani, kwani Ghana walipoteza mechi yao dhidi ya Ureno.

Hata hivyo, wote – Ghana na Ureno wameaga mashindano katika kundi lao na kuwaachia nafasi Marekani na Ujerumani. Ghana walihitaji kushinda ili kupata nafasi kwenye 16 bora.

Kwa hali ilivyo, Afrika imeingiza timu mbili kati ya tano zilizokuwa zikishiriki, ambazo ni Algeria na Nigeria. Ghana wamepoteza mechi baada ya kutokea utovu wa nidhamu na madai ya posho, ambapo wachezaji Kevin-Prince Boateng na Sulley Muntari walifukuzwa kambini na kurudishwa nyumbani saa chache kabla ya mechi hiyo kuanza..

Comments