Yanga yasajili wawili…ni Pato na Said

*Yamuacha Chuji, Luhende

SIKU mbili baada ya Simba kusajili beki chipukizi wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Joram Mgeveke, watani zao Yanga wamejibu mapigo kwa kuwanasa nyota wengine wawili wa kikosi hicho ambao ni Pato Nyongani na Said Juma.

Wawakilishi hao wa Tanzania Bara mwaka huu katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) pia imewapa mikataba mipya wachezaji wake nane ambao walikuwa wamemaliza mikataba ya kuitumikia timu hiyo.

Nyota hao waliopewa mikataba ya miaka miwili kila mmoja ni pamoja na 
nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul, Jerry Tegete, Said Bahanuzi, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Simon Msuva na Ally Mustafa ‘Barthez’.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga (jina tunalihifadhi) alisema kwamba Ngonyani anayecheza nafasi ya ulinzi amesaini mkataba wa miaka mitatu wakati kiungo mkabaji, Juma amepewa mkataba wa miaka miwili.

Kiongozi huyo alisema pia klabu yao imesajili mchezaji wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Saleh Abdallah, kwa kumpa mkataba wa miaka mitatu.

Habari zaidi kutoka Yanga zinasema kwamba klabu hiyo imesitisha maamuzi ya kumuacha kiungo wa zamani wa Taifa Stars, Nizar Khalfan, ambaye amebakiza mwaka mmoja huku ikielezwa kuwatema David Luhende na kiungo, Athumani Iddi ‘Chuji’.

“Kwa upande wa wachezaji wazawa tumemaliza, ila tumebakiza nafasi moja kwa nyota kutoka nje ya nchi,” kilisema chanzo chetu.

Alisema kuwa kikosi chao kitaingia kambini mara baada ya kuwasili kocha mpya, Mbrazil, Marcio Maximo, ambaye tayari ameshafikia makubaliano ya kujiunga na Yanga.

Juzi Yanga imempoteza kocha wake msaidizi, Boniface Mkwasa, ambaye aliondoka nchini na kuelekea Saudi Arabia kuungana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans Pluijm, katika klabu ya Al Shoalah.

Comments