Yaya, Kolo Toure wafiwa

*Mdogo wao Ibrahim aaga dunia Manchester  

Mtihani mgumu umewakumba Yaya na Kolo Toure baada ya kupata habari za kufiwa na mdogo wao, Ibrahim.

Ndugu hao wawili walipata habari hizo muda mfupi baada ya mechi yao dhidi ya Colombia Alhamisi hii.
Ibrahim (28) alifariki dunia akiwa jijini Manchester na Chama cha Soka cha Ivory Coast kimesema wao na ujumbe wote uliopo Brazil na wawili hao wapo pamoja nao katika wakati huu mgumu.

Ibrahim naye ni mwanasoka anayecheza nafasi ya ushambuliaji, ambapo amekuwa na timu ya Al-Safa SC ya Lebanon.

Tembo hao wa Afrika walishinda mechi ya kwanza dhidi ya Japan 2-1 na kufungwa na Colombia 2-1 ambapo wanahitaji ushindi dhidi ya Ugiriki Jumanne kujihakikishia wanafuzu kwa hatua za mtoano.

Wakala wa Yaya, Dimitri Seluk amesema kwamba anatumaini wawili hao watabaki kulinda hadhi ya taifa lao kwa sababu mdogo wao alikuwa shabiki mkubwa wa timu hiyo.

Yaya (31) ni mmoja wa viungo mahiri duniani na anaichezea Manchester City baada ya kupata kukipiga Barcelona wakati Kolo (33) yupo Liverpool baada ya kutoka Arsenal na City na wote ni wachezaji muhimu kwa timu ya taifa.

Comments