England majanga tupu….

England wametolewa kwenye hatua ya makundi baada ya mechi mbili tu za fainali za Kombe la Dunia.
Hii ni mara ya kwanza tangu 1958 na imetokana na Italia kufungwa na Costa Rica 1-0 usiku wa Ijumaa hii.

Wachezaji na benchi la ufundi la England walikuwa wakifuatilia mechi hiyo kwa makini katika hoteli yao jijini Rio.

Pamoja na Italia kuwa ‘wabaya’ wao kwa kuwafunga na pia kuwatoa kwenye michuano iliyopita ya Ulaya, walikuwa wakiwaombea washinde mechi zote mbili zilizokuwa zimebaki.

Hata hivyo hesabu hazikusimama upande wao, kwa sababu Costa Rica sasa wamefikisha pointi sita baada ya kuwafunga Uruguay na Italia.

Kwa upande mwingine, Italia na Uruguay kila mmoja ana pointi tatu kwa kushinda mechi moja na kupoteza moja, na ndio watakutana kwenye mechi ijayo.

England wangeweza kufuzu ikiwa mechi ingeweza kumalizika bila yeyote kupata pointi baina ya wawili hao, kisha England wawafunge Costa Rica katika mechi ya mwisho.

Lakini ilivyo sasa ni kwamba ama Uruguay au Italia watapata pointi moja na kufikisha nne na kuungana na Costa Rica waliokuwa wakichukuliwa ni wasindikizaji lakini sasa wameshafuzu kwa hatua za mtoano.

Timu nyingine zilizokwishaaga mashindano hayo baada ya mechi mbili tu ni Cameroon, Australia na Hispania. 

Comments