Uholanzi wawalowesha Hispania

 

*Mabingwa watetezi walala 5-1

 

Ilikuwa vigumu kuamini lakini ndivyo ilitokea kwa Uholanzi kuwakandika mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Hispania mabao 5-1.

 

Vijana wa Vincente del Bosque walikuwa katika hali mbaya, ambapo hata bao lao moja lilitokana na penati, David Silva akakosa nafasi muhimu na kutoa nafasi kwa wapinzani wao.

 

Wadachi wamelipiza zaidi ya kisasi kwani timu mbili hizi zilikutana kwenye fainali katika michuano iliyopita 2010 nchini Afrika Kusini na Hispania wakatoka na ushindi wa 1-0.

 

Walikuwa Hispania waliotangulia kupata bao usiku wa Ijumaa hii katika Arena Fonte Nova kwa penati ya Xabi Alonso baada a Diego Costa kuchezewa vibaya lakini mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie akasawazisha kwa kichwa kabla ya mapumziko.

 

Winga wa Bayern Munich, Arjen Robben alipachika bao la kuongoza dakika 10 za mwanzo wa kipindi cha pili kutokana na mpira wa adhabu wa Wesley Sneijder kabla ya Van Persie kumpokonya mpira kipa Iker Casillas na De Vrij kuandika bao la nne huku Robben ambaye hakuchoka akikomelea msumari wa mwisho kwenye jeneza la Hispania.

 

Hispania kama bingwa mtetezi hakuwa na kawaida ya kufungwa zaidi ya mabao manne japokuwa katika mechi ya kimataifa dhidi ya Scotland walikubali kichapo cha mabao 6-2 Juni 1963.

 

Katika michuano ya Kombe la Dunia, ni mara moja tu Hispania walilala kwa idadi kubw aya mabao (1-6) dhidi ya Brazil 1950. Uholanzi wameshika nafasi ya pili katika michuano hii kwa mara tatu, na wanaelekea kwamba safari hii wamedhamiria kufanya kweli.

 

Washabiki wa Uholanzi katika mashindano haya walikuwa wachache kuliko ilivyokuwa siku zilizopita, ikionesha kukatishwa kwao tamaa na timu kutoweza kunyakua kombe hili.

 

Diego Costa ambaye amezaliwa Brazil, akakataa kuwachezea na kuwachezea Hispania alizomewa na hakuweza kufanya la maana, akatolewa na kumwacha Fernando Torres mbele ambaye hakufurukuta.

Comments