“LIGI KUU BARA” TAYARI IMESHAANZA

 

Ndicho unachoweza kusema kwa urahisi tu pale unapopata nafasi ya kutembelea viwanja mbalimbali vya mitaa ya jiji la Dar es salaam. Huu ni muda wa mapumziko kwa wachezaji wetu kutokana na ligi kuu kumalizika lakini habari iko tofauti kabisa na unavyofikiria.

 

Wachezaji wetu wanacheza mpira kwa miezi yote 12 ya mwaka, majuma 57 na siku 365. kiungo mshambuliaji wa timu ya Coastal Union, Haruna Moshi maarufu kama Boban na beki Juma Nyosso ni moja kati ya wachezaji watakaokipiga kwenye fainali ya kugombea Ng’ombe jumapili hii.

 

Katika uwanja wa Benjamini mkapa uliopo mitaa ya Kariakoo, kutakuwa na mechi ya fainali itakayo zikutanisha timu za Faru Jeuri ya Vingunguti dhidi ya Santiago Chile ya Buguruni.

Festo Thomas, meneja wa timu ya Faru, amesema kuwa tayari kuna uwezekano wa wachezaji wengine wa ligi kuu kuweza kuongezwa kwenye kikosi chao na aliowataja ni Uhuru Suleiman, Salumu Machaku, Shabani Dihile, Godfrey Taita, Nurdin Bakari, Salumu Sued na David Luhende.

 

Hii ndiyo hali halisi ya wachezaji wetu pale ligi kuu inapokuwa ama imesimama au imemalizika. Kama unaweza kwenda kwenye fainali ya kushindania Ng’ombe na ukawashuhudia wachezaji zaidi ya 10 wa ligi kuu, kunatofauti gani na kusema ligi imeshaanza?

 

Hivi karibuni daktari wa timu ya Yanga aliweka wazi kuwa, klabu hiyo haitohusika na matibabu ya mchezaji yoyote yule ambaye atapata majeruhi kwenye mechi hizo za mchangani maarufu kama ndondo.

Kwa upande wa pili, katibu mkuu wa timu ya Mbeya City, bwana Emmanuel Kimbe, ametoa tamka zito kwa mchezaji yoyote wa timu hiyo atakayeumia kwenye mechi hizo za mchangani kuwa atakuwa amejiondoa rasmi kwenye timu yao kwani hawatomuhitaji tena.

Comments