David Luiz rasmi PSG

David Luiz sasa ni mchezaji rasmi wa mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG).
Mbrazili Luiz (27) atachezea klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano baada ya kutopewa nafasi ya kutosha kucheza na klabu yake ya Chelsea.

 

Inadaiwa kwamba mchezaji huyo amenunuliwa kwa pauni milioni 40 licha ya PSG kuwekwa kwenye kitabu cheusi kutokana na kushindwa kuwianisha mapato na matumizi ya timu.

“Tangu mawasiliano ya kwanza na PSG nilifurahishwa na klabu hii sana,” Luiz aliiambia tovuti ya klabu hiyo.
Luiz alisajiliwa kutoka Benfica Januari 31, 2011 kwa ada ya pauni milioni 21 na alikuwa mchezaji tegemeo hadi alipoanza kuachwa benchi na kocha Jose Mourinho.

Amechezea klabu hiyo mechi 143 katika mashindano yote na kufunga mabao 12. Alikuwa mmoja wa wachezaji waliofunga penati katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi ya Bayern Munich na Chelsea kutwaa kombe hilo 2012.

 

Luiz amekiri kwamba kwake PSG ni klabu mpya na kwamba ni hatua mpya katika maisha yake na anasubiri kwa hamu kuichezea ili aoneshe kile anachoweza kufanya.

Ameondoka Chelsea akiwa bado na mkataba wa miaka mitatu, kwani alijipiga kitanzi cha miaka mitano Septemba 2012
Januari mwaka huu, Chelsea walitumia pauni milioni 12 kumsajili beki wa kati wa aina ya Luiz kutoka klabu ya St Etienne, Kurt Zouma.

 

Jijini Paris, Luiz ataungana na mchezaji mwenzake wa Brazil, Thiago Silva ambaye pia akiwa mlinzi alisajiliwa kwa ada kubwa kutoka AC Milan ya pauni milioni 36.

Posted under:  All Articles

Tags:  ,

Comments