Barcelona wamchana Fabregas

 

Siku moja tu baada ya Chelsea kumsajili Cesc Fabregas, klabu yake ya zamani ya Barcelona wamemchana.
Taarifa ya klabu hiyo ya Hispania inasema kwamba kiungo huyo aliyekuzwa kwenye akademia yao ya La Masia ameshuka kiwango.

Kwamba baada ya kuondoka 2003 na kurudi Barca 2011, Fabregas alikuwa vizuri kana kwamba hakuwa ameondoka, lakini kadiri muda ulivyokwenda alishindwa kuwika.

Barcelona wanasema kwamba nahodha huyo wa zamani wa Arsenal anayedaiwa kusajiliwa kwa pauni milioni 30 na Chelsea, alishuka hatua kwa hatua kiasi cha kutoamini kama ndiye aliyekuwa akichanua hivyo kabla.

Wakamchagiza Fabregas (27) kwa jinsi alivyocheza katika nusu ya pili ya msimu uliomalizika hivi karibuni, ambapo timu yake hiyo haikupata taji lolote.

“Amekuwa akishuka kiwango kila msimu klabuni hapa …mchango wake ulipungua na kuwa mdogo sana kadiri msimu ulivyokuwa ukielekea ukingoni.

“Akabadilika kutoka mtu aliyekuwa akiunganishwa kwenye mashambulizi, akifunga mabao na uchawi wake ukageuka ambapo kwa sababu mbalimbali hakuwa tena wa msaada kwetu,” ikasema taarifa hiyo ya Barca ambayo haikutarajiwa kwa mtu aliyekuwa muhimu sana kwao tangu kitambo.

Fabregas yupo na timu yake ya taifa ya Hispania nchini Brazil, na klabu yake ya zamani ya Arsenal walikataa kutumia upendeleo kwao ulio kwenye mkataba wake kumrejesha Emirates, kwani inaona ina viungo wazuri kuliko yeye.

Anatarajiwa kuziba pengo la Frank Lampard aliyehitimisha miaka yake 13 Stamford Bridge kiangazi hiki na anatarajiwa kwenda kucheza Marekani.

 

Comments