Man United yawakataa Cavani, Fabregas

*Mancini aacha kazi Galatasaray

Manchester United wamejitoa katika mbio za kuwasajili Edinson Cavani wa Paris Saint-Germain (PSG) na Cesc Fabregas wa Barcelona.
Bosi mpya wa United, Louis van Gaal amesema kwamba hana nia ya kuwasajili wachezaji hao kwani hawapo kwenye mipango yake ya msimu ujao.

Cavani na Fabregas wanazihama klabu zao kwa sababu tofauti, Cavani akiwa hataki kuwa nyuma ya Zlatan Ibrahimovic huku Fabregas aliona atasugua benchi msimu ujao.

Man U walimtaka Fabregas tangu msimu uliopita ambapo kocha wao wa zamani, David Moyes alishindwa katika ombi lake majira ya kiangazi yaliyopita.

Kadhalika alisafiri mara tatu kwenda Paris kumtazama Cavani akicheza na aliposema anataka kuhama msimu huu, United walionesha nia lakini sasa wameghairi.

Cavani alijiunga PSG kwa ada ya pauni milioni 55 kutoka Napoli ya Italia na sasa anauzwa kwa pauni milioni 60, na anataka mshahara wa pauni 300,000 kwa wiki, kiasi ambacho Ofisa Mtendaji Mkuu wa United, Ed Woodward amesema hawezi na hataki kumlipa. Wayne Rooney analipwa kiasi hicho.

Hata hivyo, Cavani alishasema kwamba hataki kuchezea klabu ambayo haishiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kama Man U. 
Arsenal wapo kwenye mpango wa kumsajili na inadaiwa kwamba Kocha Arsene Wenger yupo kwenye mazungumzo na maofisa wa PSG ili kuboresha safu yake ya ushambuliaji.

Woodward pia amesema ameshindwa katika kumsajili Fabregas ambaye ikiwa Arsenal hawatamchukua, atakwenda Chelsea kwa pauni zaidi ya milioni 40.

United wanasubiri kupokea ofa kutoka Benfica ya Ureno; Juventus na Inter Milan za Italia kwa ajili ya winga wao ambaye hawamtaki, Nani na wanatafuta pa kumpeleka kiungo Mbrazili Anderson ili kupunguza gharama za mishahara msimu ujao.

Comments