KIPA WA YANGA KUTUA NDANDA FC

Said Mohamedi ni mlinda mlango wa zamani wa timu ya Dar es Salaam Young Africans ambaye kwa sasa anakipiga na wakatamiwa wa Manungu kule mkoani Morogoro, timu ya Mtibwa Sugar. Habari zilizoenea ni kwamba, kipa huyo anawindwa kwa udi na uvumba na watoto wa Mtwara, timu ya Ndanda Fc.

Ndanda Fc wanataka kujiimarisha kwa kuongeza watu wenye uzoefu kikosini mwao na Said Mohamedi ni mchezaji wanaodhani atawafaa. Said Mohamedi bado anamkataba na timu yake hivyo, klabu inayomuhitaji ni lazima wamalizane na Uongozi wa timu hiyo inayonolewa na kocha Mecky Mexime.

Kwa upande wa pili, Klabu ya Simba imeanza mazungumzo ya kumnasa kiungo mshambuliaji wa klabu ya APR ya nchini Rwanda, Jeas-Baptiste Mugiraneza. Huyu ni fundi anayekipiga kwenye timu ya taifa ya Rwanda maarufu kwa jina la Amavubi. Endapo Simba watafanikiwa kumnasa, atakuja kusaidiana na kiungo wa kutegemewa wa timu hiyo, Jonas Mkude.

Kwa mujibu wa kanuni za shirikisho la soka Tanzania, kila klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi watano wakigeni ambapo mpaka sasa, tayari Simba inawachezaji watatu na imebakiwa na nafasi mbili tu.

Wachezaji wa kigeni waliopo ni beki Joseph Owino na Donald Musoti wote kutoka nchini Kenya na mshambuliaji Amisi Tambwe kutoka nchini Burundi. Kwa idadi hiyo, inafanya timu ya Simba kubakiwa na nafasi mbili tu kwa ajili ya wachezaji wa kigeni.

Kwa kumalizia, klabu ya JKT Ruvu tayari imekamilisha usajili wa beki Mohamedi Fakhi ambaye msimu uliopita alikuwa na timu ya Ashanti United ambayo ilishuka daraja. Fakhi alijiunga na Ashanti United kwenye dirisha dogo la usajili mwaka huu akitokea klabu ya Zimamoto ya huko Zanzibar.

Comments