Chelsea wamsajili Fabregas

Nahodha na kiungo wa zamani wa Arsenal, Cesc Fabregas amejiunga na klabu pinzani ya London ya Chelsea.

Fabregas (27) amesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano baada ya Arsenal kutoonesha nia ya kumrejesha London Kaskazini ambako wangeweza kwa mujibu wa mkataba wao wa mauzo.

Mhispania huyo amekaa Barcelona kwa miaka mitatu baada ya kuwa Arsenal lakini pia alianzia maisha ya soka Barca katika akademia yake ya La Masia.

Akiwa Arsenal alifunga mabao 50 katika mechi 305 wakati kwa Barca alifunga mabao 35 katika mechi 129, na amerejea England akisema kulikuwa na kitu hajakamilisha kwenye ligi hii maarufu kuliko zote duniani.

“Nilitafakari kwa makini ofa nyingine zote na Chelsea ndilo chaguo langu bora zaidi,” akasema Fabregas anayedhaniwa kwamba ada yake ya uhamisho ni kwenye pauni milioni 30.

Anaingia kuziba pengo la Frank Lampard ambaye anaondoka klabuni hapo baada ya miaka 13 ya kucheza wakati ambapo Kocha Jose Mourinho anahangaika kukamilisha usajili wa mshambuliaji Diego Costa wa Atletico Madrid.

Fabregas yupo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Hispania ambako amecheza mara 89.

Arsenal wameamua kutomsajili Fabregas kwa sababu kwenye eneo la kiungo wanao wachezaji wengi wazuri kama Jack Wilshere, Aaron Ramsey, Mesut Ozil, Mikel Arteta na Alex Oxlade-Chamberlain.

Comments