KAPOMBE AZIGONGANISHA AZAM, SIMBA

BEKI kiraka wa timu ya taifa, Shomari Kapombe amezua zogo baada ya uongozi wa klabu ya Simba kusema haupo tayari kupokea kiasi kidogo cha fedha kutoka Azam.

Klabu ya Azam imekuwa kwenye mchakato wa kumsajili beki huyo wa zamani wa Simba, ambey alikwenda nchini Ufaransa katika klabu ya AS Cannes kufanya majaribio, lakini alishindwa kudumu hivyo kurejea nchini.

Hata hivyo, klabu ya Azam imesema kuwa wenzao wa Simba wanadanganywa kwa kiwango kikubwa na wakala Dennis Kadito kuhusu kiwango halisi cha manunuzi ya mchezaji Shomari Kapombe.

Azam wamesema kuwa wamefanikiwa kuinasa saini ya Shomari Kapombe kwa Euro 43,000, ambapo klabu ya AS Cannes iliwaelekeza wailipe Simba 40% ya dau hilo, kisha 20% wamlipe wakala Dennis Kadito.

Kwa upande wao klabu ya Azam imesema kuwa itahakikisha inafuata maelekezo yote juu ya mchakato wa malipo, licha ya klabu ya Simba kudai fedha zaidi ya kile wanachostahili kulipwa.

Kabla ya kumnunua Kapombe, klabu ya Azam iliwasiliana na wakala Dennis Kadito, lakini alidai dau kubwa zaidi hali ambayo iliwalazimisha viongozi wa Azam kuzungumza na wenzao wa AS Cannes.

“Sisi tunafahamu kuwa Shomari Kapombe ni mchezaji aliyekuwa na mkataba na AS Cannes, tulichofanya ni kumnunua kutoka huko na tukapewa maelekezo yote ya mchakato wa malipo, hivyo tutawalipa Simba na wakala Dennis Kadito,” kilisema chanzo cha habari hizi ambacho hakikupenda kutajwa jina.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa klabu ya Simba ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini , Ismail Aden Rage aliweka wazi kuwa hawana mpango wa kupokea fedha chini ya Euro 43,000 zitakazolipwa na Azam ili kumnasa Shomari Kapombe.

Comments