Wilshere: Pirlo haendi popote

Kiungo wa Timu ya Taifa ya England, Jack Wilshere anasema kwamba watahakikisha wanamkaba vilivyo Andrea Pirlo wa Italia.
Mchezaji huyo wa Arsenal anasema kumnyima fursa Pirlo ya kuwasumbua, akitambulika kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa katika mashindano hayo, kutawasaidia England kuibuka na ushindi dhidi ya Italia.

England wanacheza na wababe wao hao katika Jiji la Manaus Jumamosi hii. Pirlo (35) aliwatesa sana England kwa pasi zake, Italia walipowafunga England kwa penati katika nusu fainali za Euro 2012.
Wilshere (22) anasema wametumia mechi zao za majaribio kujiandaa kudhibiti mbinu zote za Pirlo na wenzake.

“Tunajua umri wake unakwenda lakini tunafahamu fika kwamba bado ana kiwango cha hali ya juu kwa hiyo tumejiandaa kumkabili vilivyo,” anasema Wilshere.

Akimzungumzia kipa wa Italia, Gianluigi Buffon mwenye umri wa miaka 36, Wilshere anasema itafika mahali kwenye mechi watamshosha na ataachia tu mabao.
Wilshere anasisitiza kwamba England hawawaogopia Italia wala hali ya hewa, japokuwa awali walikuwa na hofu. Kwamba hivi sasa wameshajiweka sawa kimashindano kwa kila hali.

England hawajapata kuvuka hatua ya robo fainali katika mashindano mengi miaka ya karibuni. Walitwaa Kombe la Dunia mara moja tu, nayo ilikuwa 1966 kabla wachezaji wote walio kwenye timu hiyo hawajazaliwa na kocha wao, Roy Hodgson alikuwa kijana.

Comments