Blatter: Harufu ya ubaguzi Qatar

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter amejikusanya na kujibu mapigo ya rushwa inayoliandama shirikisho hilo na kusema tuhuma zote zina harufu ya ubaguzi.
Blatter anadai kwamba yote yaliyoelekezwa kwa wajumbe wa mkutano wa Fifa, Kamati ya Maandalizi ya Kombe la Dunia 2022 ya Qatar na Mohammed bin Hammam yananuka ubaguzi mtupu.

Ameng’aka na kudai msukumo wote wa tuhuma zina sinikizo la uonevu na ubaguzi wa rangii dhidi ya wajumbe wa shirikisho lake, lakini pia kwa Waarabu na Waafrika.
Blatter (78) alikuwa akizungumza jijini Sao Paulo, Brazil na wajumbe wa Fifa kutoka Asia, akasema suala hilo litajadiliwa kwenye Baraza la Fifa Jumanne na Jumatano hii na litafungwa.

Badala ya kujibu shutuma moja baada ya nyingine, Blatter amekimbilia kusema kwamba lazima Fifa ipambane na kila kitu chenye harufu ya kutenganisha watu isivyo halali.
Mwaka 2010 mkutano wa Fifa uliichagua Qatar kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia 2022, na sasa kuna tuhuma kwamba mamilioni ya dola yalitolewa na Bin Hammam kwa wajumbe ‘kununua’ uenyeji huo.

Pamoja na mambo mengine, Bin Hammam aliyekuwa Makamu Rais wa Fifa, anadaiwa alitoa fedha kwa wajumbe wa Afrika, akiwamo Mwenyekiti wa CAF, Issa Hayatou, tiketi za Kombe la Dunia, suti, kugharamia malazi kwenye hoteli za kitalii Doha kwa wajumbe kadhaa na mengine mengi.

Kwa mshangao wa wengi, Fifa ilipitisha mashindano yafanyike nyakati za majira ya joto ambapo huwa na joto kali sana. Qatar waliwashinda Australia, Japan, Korea Kusini na Marekani.
Mwanasheria Michael Garcia anaongoza jopo la uchunguzi huru juu ya mlungula na mchakato huo na anatarajiwa kutoa ripoti yake katikati ya mwezi ujao wa Julai.

Comments