KUELEKEA KOMBE LA DUNIA 2014

Cameroon wamaliza mzozo wa posho

Hatimaye Cameroon wamemaliza mzozo juu ya posho za wachezaji wao ambao tayari wamefunga safari kwenda Brazil kwa fainali za Kombe la Dunia.

Mzozo huo umetia doa soka ya Afrika kwa mara nyingine, kwa namna ya pekee ikiikumba tena nchi hiyo ambayo ilikuwa katika mvutano kabla ya kufuzu.

Kikosi hicho kinamjumuisha mfungaji aliyemaliza mkataba wake Chelsea, Samuel Eto’o, ambapo wachezaji walikataa kupanda ndege Jumapili asubuhi.

Baada ya jitihada za kila namna, hatimaye Shirikisho la Soka la Cameroon lilifanikiwa kumaliza mtanziko huo kwa mkutano wa dharura.
Timu hiyo ilitarajiwa kuondoka Younde kwa kuchelewa saa 12 ili wawasili jioni ya jana Jumapili nchini Brazil.

Kocha wa timu hiyo, Volker Finke alisema awali kwamba wachezaji walikuwa wakilalamikia posho ya pauni 61,000 ambayo wangelipwa kwa kushiriki kwenye michuano hiyo, wakidai hakitoshi.

Baada ya makubaliano yaliyomaliza mvutano wao, Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon, Joseph Owona alisema kwamba hakuna tena hata chembe ya mvutano kwenye ujumbe unaokwenda kupeperusha bendera ya Simba Wasiofugika.

Owona alisema kwamba wameamua kuwa wawazi, hakuna tena tatizo lakini akakazia kuwa uhamasishaji sasa unatakiwa ili timu ifanye vizuri.
Cameroon wapo katika kundi ‘A’ na wenyeji Brazil pamoja na Croatia na Mexico.

Comments