Abramovich kuwatosa Chelsea?

*Adaiwa kutaka kununua Real Mallorca

Kuna habari kwamba mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich anataka kuhamishia himaya yake nchini Hispania.
Abramovich ambaye amekuwa mmiliki wa Chelsea tangu 2003 inasemakana anatafuta jinsi ya kununua klabu ya soka ya Real Mallorca inayocheza Ligi Kuu ya Hispania.

Bilionea huyo wa Kirusi anaelekea ama kuwachoka Chelsea au kuna kitu anakikimbia, na umiliki wa klabu mbili Ulaya unawezekana lakini hazitatakiwa zote kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).

Ikitokea kweli atawanunua Mallorca na kuwafadhili hadi wafike UCL na Chelsea wawe huko, itabidi aache umiliki wa klabu moja
Pamekuwapo nadharia kwamba Abramovich anayejulikana kwa kuajiri na kufukuza makocha ovyo ovyo, amechoshwa na kanuni za fedha zinazowabana Chelsea katika usajili.

Kwingineko inasemwa kwamba tajiri huyo mwenye makazi yake London amechoka maombi ya Jose Mourinho ya fedha kwa mambo mbalimbali lakini kwa utani kwenye korido inasemwa kwamba boti yake ya kifahari (yoti) itatia nanga uzuri zaidi  kule Mallorca kuliko London.

Fununu hizi zinakuja wakati ambapo Chelsea wanaonekana kugeuka klabu ya kuuza wachezaji, ambapo baada ya kumuuza kwa bei kubwa David Luiz, kuachana na Samuel Eto’o, inadaiwa hata Eden Hazard atauzwa.

Nadharia nyingine juu ya Abramovich kutaka kuachana na Chelsea inasema kwamba anaweza hata kuiuza klabu hiyo.

Kwamba sababu kubwa ni kutoweza kushindana na mashehe bilionea wanaomiliki Manchester City wakati yeye alitaka awe juu ya klabu zote. Man City kutwaa ubingwa mwaka huu baada ya ule wa 2012 ni dalili kuwa wanaimarika na watakuwa tishio kubwa.

Je yawezekana kwamba Abramovich anataka sasa kuelekeza nguvu zake Hispania akapambane na Barcelona na Real Madrid kwa kuwapandisha Real Mallorca kutoka nafasi za chini walimo? Soka ina mengi, na lolote lawezekana; pengine mwisho wa himaya ya Roman kwa Chelsea unakaribia.

Comments