Wanachama Simba waenda FIFA….

Wasema Malinzi anambeba Wambura!

WANACHAMA watano wa Simba wametuma barua katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) wakimshtaki, Rais wa Shirikisho la Mchezo huo Nchini (TFF), Jamal Malinzi, wakidai ‘anampendelea’ aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Rais katika Uchaguzi Mkuu wa Simba, Michael Wambura.

Kamati ya Uchaguzi ya Simba ilimuengua Wambura katika mchakato wa uchaguzi kutokana na mgombea huyo kusimamishwa uanachama tangu Mei 5 mwaka 2010 kufuatia kufungua kesi kwenye Mahakama ya Kisutu yenye namba 100/2010 akiushitaki uongozi uliokuwa madarakani wakati huo.

Wanachama hao watano wa Simba waliowasilisha malalamiko yao FIFA dhidi ya Malinzi ni pamoja na  Masoud Hassan mwenye kadi namba 0500, Salehe Shahame (05596), Frank Pastoli (01288), Rajab Mtitu (01146) na Ally Mkumba (02519).

“Wambura ana kesi ya kimaadili na Kamati za Uchaguzi hazina mamlaka ya kuziamua kwa sababu kupeleka masuala ya soka kwenye mahakama za kawaida ni kosa kama katiba ya FIFA inavyoeleza,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Wanachama hao wa wadai katika barua hiyo iliyoandikwa Juni 3 mwaka huu kuwa Malinzi anadaiwa kuishinikiza Kamati ya Rufaa na Kamati ya Maadili kumrejesha Wambura kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi licha ya kufanya kosa hilo linaloenda kinyume na katiba ya Simba, TFF na FIFA.

Katika barua yao wameeleza kwamba tayari Malinzi ameshatoa maelekezo kwa kamati ya Rufaa imrejeshe mgombea huyo kwenye uchaguzi huo.

Katika barua hiyo wanachama hao wametuma nakala kwa viongozi wanaoshughulika na masuala ya uanachama ambao ni Thiery Reganass, Primo Corvaro na Ashford Mamelodi.

Malinzi aliliambia gazeti hili jana kwamba yeye na TFF haina nia ya kuingilia mchakato wa uchaguzi wa Simba ambao unatarajia kufanyika Juni 29 mwaka huu.

Kiongozi huyo wa juu alisema kwamba shirikisho hilo inachofanya ni kuhakikisha katiba na kanuni za uchaguzi kwa wanachama wake zinafuatwa.

Tayari kamati ya Rufaa ya Uchaguzi imesema kuwa itasikiliza rufaa ya Wambura Jumatatu Juni 9.

Comments