England wana mtihani mkubwa

England wamekwenda sare ya 2-2 katika mechi ya kujipima nguvu dhidi ya washiriki wenzao kwenye fainali za Kombe la Dunia, Ecuador.

Katika mechi hiyo, kiungo wa England na Arsenal aliyetoka kwenye mapumziko ya majeruhi hivi karibuni, Alex Oxlade-Chamberlain aliumia goti na kuna wasiwasi kwamba akashindwa kuiwakilisha nchi.

Hata hivyo, hatima yake itajulikana baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina na madaktari. Tatizo jingine ambalo England walipata ni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa mchezaji wao chipukizi, Raheem Sterling kwa kumchezea vibaya Antonio Valencia ambaye pia alitolewa nje.

Wote wawili hawataruhusiwa kucheza kwenye mechi za mwisho za kujifua kabla ya kuanza kwa mashindano hayo Alhamisi ijayo nchini Brazil. Valencia anayechezea Manchester United naye alitolewa nje kwa kukurupuka na kutaka kumkunja Sterling.

England walionekana kutokuwa wazuri kwenye ulinzi lakini chipukizi wa Everton, Ross Barkley alicheza vizuri. Ecuador walitumia udhaifu wa ngome ya England kupata bao la kwanza kupitia kwa Enner Valencia kabla ya Wayne Rooney kusawazisha kabla ya nusu ya kwanza kumalizika.

Mshambuliaji wa Southampton aliyesajiliwa na Liverpool kwa msimu ujao, Rickie Lambert  kwa pauni milioni nne alifunga bao la pili lakini likasawazishwa na Michael Arroyo aliyetokea benchi.

Kocha Roy Hodgson wa England alisema litakuwa pigo kubwa iwapo watampoteza Oxlade-Chamberlain (20) kwa sababu yupo kamili katika mipango yake. England wapo kwenye kundi gumu, wakiwa na Italia, Costa Rica na Uruguay.

Comments