Mtoto wa Pele jela miaka 33

Wakati Ulimwengu wa Soka ukitazama mbele kwa ajili ya Kombe la Dunia, gwiji wa soka kihistoria, Pele amepata pigo kubwa baada ya mwanawe
Edinho Edson Cholbi do Nascimento kutupwa jela miaka 33.

Edinho (43) ametiwa hatiani kwa makosa ya jinai ya kutakatisha fedha zilizotokana na mauzo ya dawa za kulevya.

Edinho alipata kuchezea Santos akiwa kipa katika klabu ya zamani ya baba yake alikotokea pia Neymar wa Barcelona na baada ya kufikishwa mahakamani alikiri makosa yake hayo.

Aliwahi kukamatwa mwaka 2005 na kutupwa ndani katika operesheni ya kusambaratisha genge la watumiaji, wasafirishaji na wauzaji wa mihadarati katika Jiji la Santos kabla hajaachiwa.

Pele alisema mwaka 2006 kwamba Mungu akipenda haki ingetendeka na kwamba hapakuwa hata tone la ushahidi dhidi ya mwanawe huyo.

Hata hivyo, kwa sasa Edinho atakuwa huru kwa sababua meamua kukata rufaa licha ya kukiri kununua mihadarati anasema hakuwa akifanya kazi na genge hilo hatari.

Mahakama ya Praia Grande ilitoa adhabu kama hiyo kwa washitakiwa wengine watatu na kuamuru mali zao zote zikamatwe na kutaifishwa, zikijumuisha jumla ya magari 100.

Pele ambaye ni Balozi wa Kombe la Dunia na linafanyika nchini mwake, atatakiwa kushughulikia suala la mtoto wake sambamba na mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani.

Brazil imeshaandamwa kwa kushindwa kukamilisha viwanja kwa wakati, huku baadhi ya wananchi wakiandamana kupinga matumizi makubwa ya fedha kwenye soka wakati hali zao ni mbaya.

Edinho alistaafu soka 1999 wakati baba yake, Pele (73) anachukulia kama moja ya nembo muhimu zaidi za soka duniani.

Comments