Wachezaji lazima waimbe Wimbo wa Taifa

Wachezaji wanatakiwa kujua na kuimba Wimbo wa Taifa kwa umakini na nguvu ili kuonesha uzalendo kwa taifa lao.

Kocha wa Timu ya Taifa ya England, Roy Hodgson amesema anatarajia wachezaji wake wote kuweza kuimba wimbo wao nchini Brazil.

Hodgson anasema ni fahari kubwa kwa wachezaji kujua wimbo wa taifa lao na kuonesha uzalendo kwa kuimba vizuri. Uingereza wana wimbo wao unaoitwa ‘God Save The Queen’.

Pamekuwa na matukio kadhaa Ulaya na Afrika pia ambapo wachezaji hawajui wimbo wa taifa na hushindwa kuuimba, wakiachia bendi kupuliza matarumbeta.

Wachezaji wanatakiwa kutulia, kuweka mikono kwenye eneo ilipo mioyo yao kifuani na kuimba neno moja baada ya jingine la wimbo wa taifa huku bendera ya nchi husika zikipepea.

England ilichukua hatua za makusudi kwamba wachezaji wajiandae, hasa kwa kuwa kuna wengi wapya kwenye kikosi hicho, baadhi wakiwa na asili ya nchi nyingine hivyo wanaweza kuwa hawaujui vyema.

England wapo Miami, Marekani wanakofanya mazoezi ya mwisho mwisho kabla ya kwenda Brazil na Ijumaa waliwafunga Peru 3-0 kwenye mechi ya kujipima nguvu.

England wamekuwa wakifanya vibaya kwenye michuano mikubwa, mara nyingi wakiishia hatua za robo fainali.

Comments