Rickie Lambert huyooo Liverpool

Liverpool wanakamilisha usajili wa mshambuliaji wa Southampton na Timu ya Taifa ya England, Rickie Lambert.

Tayari amefaulu kwenye vipimo juu ya afya yake, ambapo klabu hizo mbili zimekubaliana ada ya kwenye pauni milioni nne na nyongeza nyingine kadhaa.

Lambert (32) anatarajiwa kuidhinishwa rasmi Jumatatu hii akiwa ameshaondoka kwenda Miami, Marekani na timu ya taifa kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia.

Mchezaji huyu aliyezaliwa Liverpool atakuwa na mkataba wa miaka miwili na alipata kucheza Anfield akiwa kwenye timu ya vijana. Ijumaa alikuwa benchi wakati England walipowachapa Peru 3-0 kwenye mechi za mazoezi.

Msimu huu amefunga mabao 14 katika mechi 39. Kwa ujumla amefunga mabao 117 katika mechi 235 tangu alipojiunga Southampton akitoka Bristol Rovers mwaka 2009.

Mkataba wake Saints ulikuwa bado miaka miwili lakini klabu mbili hizo zimekubaliana, ambapo mchezaji wa zamani wa Anfield, Robbie Fowler anaamini ni hatua muhimu iliyochukuliwa na kocha Brendan Rodgers.

Januari mwaka huu Saints walikataa ofa kutoka Liverpool na West Ham kwenye usajili wa dirisha dogo. Southampton hawana kocha, baada ya mwalimu wao, Mauricio Pochettino kujiunga Tottenham Hotspur.

Liverpool bado wapo kwenye mazungumzo na wenyeji hao wa Dimba la St Mary’s kuhusu kiungo wa England, Adam Lallana (26) na yule mlinzi wa Croatia, Dejan Lovren (24).

Kadahalika Liverpool wanataka kumsajili beki wa Sevilla, Alberto Moreno (21) na wapo tayari kutoa hadi pauni milioni 16.

Southampton pia wanaendelea na mazungumzo na Manchester United wanaotaka kumsajili beki wa kushoto wa Timu ya Taifa ya England, Luke Shaw, ambaye Chelsea wanamwinda pia.

Comments