Moyes: Laiti ningepewa muda Man United

*Asema kuna ofa nyingi lakini anapumzika

Kocha wa zamani wa Manchester United, David Moyes anaamini alistahili kupewa muda zaidi kuwanoa Mashetani Wekundu hao.

Moyes (51) aliyefukuzwa kazi akiwa mwezi wa 10 katika mkataba wake wa miaka mitano, anasema Man U haiwezi kurekebishwa haraka, bali inahitaji muda.

Anasema ni bahati mbaya kwamba hakupewa muda huo, kwamba amejifunza mengi katika muda huo na kwamba aliyemsaidia tu ni Mskochi mwenzake, Sir Alex Ferguson aliyempendekeza kuvaa viatu vyake baada ya kukaa hapo kwa miaka 26.

Moyes anasema amepata ofa nzuri kutoka kwa klabu moja au zaidi lakini anafikiria kupumzika nje ya soka kwa muda badala ya kuzikubali.

Inaelezwa kwamba Celtic, mabingwa wa Scotland wameshamfuata kutaka azibe pengo la Mskochi mwenzake, Neil Lennon.

“Naamini nitakuwa na busara zaidi na kocha mwenye ujuzi zaidi baada ya kuwa kocha pale Old Trafford,” anasema Moyes ambaye nafasi yake inachukuliwa na Mdachi Lous van Gaal.

Moyes anasema kwamba angepewa muda angetekeleza vyema mpango wake wa muda mrefu wa kuifufua United na kwamba baada ya kuondoka alitumiwa ujumbe wa kumtakia heri na wachezaji, wakiwamo Wayne Rooney na Darren Fletcher.

Anasema Fergie alimshauri baadhi ya maeneo ya kurekebisha na kufanyia mabadiliko, mipango aliyokuwa ameshaianza lakini cha kushangaza akafukuzwa kabla hata mchakato haujafika mbali.

Kinachoshangaza katika wakati wake huo wa miezi 10 ni Man U kuvunja rekodi kwa kufanya vibaya wakati ni kikosi kile kile kilichokuwa kimetwaa ubingwa msimu uliotangulia chini ya Fergie.

Comments