Fabregas anauzwa pauni mil. 30

*David Villa atangaza kuondoka Atletico

Wachezaji wawili mahiri wa Hispania, Cesc Fabregas (Barcelona) na David Villa (Atletico Madrid) wanatarajiwa kuhama klabu zao msimu huu wa kiangazi.

Wakati Barcelona wakisema kiungo wao huyo anaweza kuondoka klabuni hapo ikiwa itawajia klabu na kitita cha pauni milioni 30.

Inaelezwa kwamba Fabregas (27) anataka kurudi kucheza kwenye Ligi Kuu ya England ambako alikuwa nahodha wa Arsenal kabla ya kurudi Barca ambako alianzia akiwa mtoto katika akademia yao ya La Masia.

Tayari Barcelona imewajulisha maofisa wa klabu zinazodhaniwa kumtaka juu ya uwapo wake. Alisajiliwa Barca kutoka Arsenal kwa pauni milioni 35 mwaka 2011 akirudi kwani alitoka Barca kwenda Arsenal 2003.

Arsenal wanatarajiwa watapenda kumchukua lakini inatambulika kwamba msimu uliopita Manchester United walitaka kumsajili wakashindwa, kwani hakuwa akiuzwa.

Kwa upande wa Villa, inaelezwa kwamba mkongwe huyo aliyefunga mabao mengi nchini Hispania ameshawaaga wenzake kwamba msimu ujao hatakuwa Atletico licha ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Villa (32) yumo kwenye kikosi cha Timu ya taifa ya Hispania na inasemwa kwamba amepata timu nchini Marekani, na mwenyewe anasema hawezi kukataa ofa yao. Amekaa msimu mmoja tu Atletico.

Amepata kuchezea klabu za Real Zaragoza, Valencia, Barcelona na sasa anaanua pazia Atletico. Inadhaniwa kwamba atajiunga na klabu ya New York City FC ya Marekani inayomilikiwa na wale wale wanaoimiliki Manchester City.

Comments