Eto’o aitaka Arsenal

*Asema Mourinho ni kibaraka

Mshambuliaji wa kati wa Cameroon, Samuel Eto’o ametangaza kutaka kujiunga na Arsenal ili amwoneshe Jose Mourinho kwamba bado wamo na amwaibishe watakapokutana.
Eto’o amekuwa katika majibizano na kocha wake huyo wa Chelsea, ambapo Mourinho amekuwa akimbeza kwamba hawezi kufunga mabao naye akamjibu kwa ishara uwanjani akiigiza kama mzee baada ya kufunga bao.

Eto’o amesema ana uwezo mkubwa wa kupachika mabao ambapo amedai kwamba kocha wake wa sasa, Mourinho ni kibaraka tu na hajui analolisema.
Mourinho alirekodiwa bila kujua akisema kwamba anadhani umri wa mshambuliaji huyo wa Simba Wasiofugika ni mkubwa kuliko inavyodaiwa, na majuzi Eto’o alimshambulia kocha huyo akisema ni mpuuzi.

“Wawakilishi wa Eto’o wameshaasiliana na Arsenal kuwajulisha kwamba mwanasoka huyo anaweza kupatikana kipindi hiki kama mchezaji huru hivyo wamchukue bila ada na kwamba kipaumbele chake namba moja ni kwenda Emirates,” mtu wa karibu na Eto’o amesema.

Eto’o mwenye umri wa miaka 32 amekuwa akidaiwa na Mourinho kwamba huenda anazidi miaka 35. Bosi wa zamani wa Eto’o katika timu ya taifa, Claude Le Roy amesema kwamba Eto’o amechukizwa sana na maneno ya Mourinho ya kumbeza.

Le Roy anasema kwamba Eto’o anaamini kwamba anaweza kufunga mabao mengi katika kipindi chote cha msimu na amedhamiria kuondoka Chelsea kwenda kuonesha ujuzi huo sehemu nyingine, hasa Arsenal.

“Uzuri wangu ni kwamba naweza kufunga mabao hata nikiwa na miaka 37 kwa sababu bado nina nguvu, uwezo na maarifa, si ajabu hata nikifikisha miaka 50 … hilo ndilo suala lililopo mezani wala si mambo ya Mourinho, nataka kujitoa kabisa kwa ajili ya timu na kuwasaidia kushinda vikombe.

“Kinyume na anachosema kibaraka huyo (Mourinho) juu ya umri wangu, bado nipo fiti kabisa na najihisi buheri wa afya. Nimethibitisha kwamba naweza kufanya vyema kuliko hata chipukizi,” akasema Eto’o ambaye anakwenda kwenye Kombe la Dunia kuwaongoza Cameroon.

Eto’o ndiye mshambuliaji wa kati wa Chelsea aliyefunga mabao mengi zaidi msimu uliopita (12) wakati wenzake Fernando Torres alifunga tisa na Demba Ba manane tu. Eto’o alifunga mabao matatu (hat-trick) dhidi ya Manchester United.

Kama atajiunga Arsenal atakuwa wa msaada mkubwa kushirikiana na Olivier Giroud na kusaidia mashambulizi na zaidi sana umaliziaji wa makini na kijanja, kitu ambacho Eto’o amethibitisha kuwa nacho.

Comments