KUNA LA KUJIFUNZA KWA FRANCIS CHEKA

Unapogeuzia shingo upande wa mchezo wa masumbwi maarufu kama “ndondi” hapa nchini, utakutana na majina ya kina Japhet Kasseba, Mada Maugo, Thomas Mashali na wengine kibao. Orodha hiyo haiwezi kukamilika pasipokuwepo jina la Francis Cheka mtoto wa mji kasoro bahari pale mkoani Morogoro.

Cheka ni moja ya vijana wakitanzania wanaopaswa kuigwa kwa namna anavyopambana katika kujitafutia maisha bora. Aliwahi kucheza pambano mwaka 1999 na kulipwa shilingi elfu 10 tu lakini, hakukata tamaa.Kadri muda na ubora wake unavyoongezeka, ndivyo thamani yake inavyozidi kupanda na kwa sasa, kupewa milioni tano hadi 10 kwa pambano moja ni kitu cha kawaida tu.

Wakati macho na masikio ya watanzania wengi yakiutazama mchezo wa soka tu, upande wa pili kuna watu kutoka fani mbalimbali tofauti na soka ambao wanaipeperusha vyema bendera ya taifa letu. Mchezo wa ndondi ni moja ya maeneo ambayo wadau wakiyatazama kwa jicho la tatu na kufanya uwekezaji, tunaweza kusonga mbele kama taifa.

Pamoja na kuwa hakupata fursa ya kupata elimu angalau ya sekondari, bado hajakata tamaa kila siku anaonyesha dhamira yake ya kutaka kujiendeleza kielimu. Ni moja kati ya vijana wachache sana wanaoweza kuwaza elimu hasa baada ya kupata fedha na umaarufu.

Bado kuna changamoto nyingi upande wa mchezo wa masumbwi hapa nchini na kubwa kuliko yote, ni ubabaishaji wa mapromota. Kumekuwa na tabia ya kukiuka mikataba waliyoingia na mabondia na wakati mwingine, kumekuwa na dhuluma na unyonyaji.

Bado wadau wengi wanahitajika kwenye tasinia hii ili kufanya mchezo huu kuweza kusambaa nchi nzima na kuwanufaisha vijana wengi wenye ndoto za kuwa kina Mike Tyson wa baadae. Mabondia wetu wanahitaji kuwa na menejimenti zenye uelewa wa kutosha juu ya kazi hiyo na isichukuliwe kama kazi ambayo anaweza kuifanya mtu yoyote.

Comments