Spurs wamtaka Kocha Pochettino

Klabu ya Tottenham Hotspurs wamefika hatua muhimu katika mazungumzo ya kumchukua Kocha wa Southampton, Mauricio Pochettino.
Spurs walio kaskazini wa London wamekuwa katika harakati za kutafuta kocha tangu walipomfukuza Tim Sherwood mapema mwezi huu.

Pochettino (42) alijiunga na Southampton Januari mwaka jana kuchukua nafasi ya Nigel Adkins aliyefutwa kazi katika klabu iliyo pwani ya kusini ya England.

Amefanikiwa kuwaongoza Saints wakamaliza Ligi Kuu ya England wakiwa nafasi ya nane na alizifunga timu kubwa kama Chelsea, Manchester City na Liverpool.

Palikuwa na maswali mengi juu ya hatima ya Pochettino hapo Southampton, hasa baada ya kuondoka kwa Mwenyekiti Nicola Cortese Januari mwaka huu.

Spurs ambao kabla ya Sherwood walimfukuza kazi Kocha Andre Villas-Boas na kabla ya hapo walimfukuza mkongwe Harry Redknapp walidaiwa kufanya mazungumzo na Kocha wa Ajax, Frank de Boer ambaye amekana kuwasiliana nao.

Pochettino ni raia wa Argentina ambaye mapema mwezi huu alisema angejadiliana na klabu juu ya hatima yake kwenye Dimba la St Mary’s ambako amebakiwa na mkataba wa mwaka mmoja.

“Ni juu ya bodi kujadili nami juu ya mwelekeo wa baadaye wa klabu msimu ujao,” Pochettino alikaririwa akisema na kuongeza kwamba hakujua lini mazungumzo hayo yangefanyika.

Pochettino ambaye hazungumzi Kiingereza amepata kuchezea klabu za Old Boys, Espanyol, PSG na Bordeaux na mara 20 kwa Timu ya Taifa ya Argentina. Amekuwa kocha wa Espanyol tangu 2009.

20140527-141200-51120181.jpg

Comments