MAMBO SI MAMBO KWA MTIBWA SUGAR

Moja kati ya timu kongwe kwenye ligi kuu ya Tanzania bara Mtibwa Sugar kutoka Manungu, Turiani kule mkoani Morogoro, wamejikuka kwenye sintofahamu kutokana na timu hiyo kuendelea kuboronga kwa mara nyingine tena kwenye ligi kuu iliyomalizika hivi karibuni.

Mtibwa Sugar walijikuta wakimaliza katika nafasi ya saba baada ya kujikusanyia alama 31 tu kutokana na michezo 26 ambayo walishiriki.Timu hiyo ilishindwa pia kutumia vema uwanja wake wa nyumbani baada ya kujikuta wakitoka sare kwenye michezo mingi ya nyumbani na kupoteza ile ya ugenini.

Taarifa za ndani kutoka katika timu hiyo zinaeleza kuwepo kwa uwezekano wa kufanyika kwa mabadiliko makubwa kuanzia kwenye benchi la ufundi mpaka wachezaji. Baada ya kocha wao Mecky Maxime kuiongoza timu hiyo kwa misimu kadhaa na kushindwa kuipeleka mbele, kuna habari za timu hiyo kumtafuta kocha mwingine.

Mtibwa Sugar ni mabingwa wa zamani wa ligi kuu Tanzania bara baada ya kutwaa ubingwa huo mara mbili mfululizo. Walifanya hivyo mwaka 1999 na 2000 na sasa, hawaonekani kama watakuja kufikia tena mafanikio hayo kama mabadiliko makubwa hayatofanyika.

Watoto hao wa Morogoro ndiyo walikuwa timu pekee iliyokuwa ikitoa changamoto kwa timu kongwe hapa nchini za Simba na Yanga kablya ya ujio wa Mbeya City na Azam fc. Lakini kwa sasa wanaonekana kupotea na moja ya sababu, itakuwa ni kuondokewa kwa wachezaji wake muhimu kila msimu unapomalizika.

Tayari kwa sasa kunahabari za beki kisiki wa timu hiyo Salvatory Ntebe kujiunga na Ruvu Shooting huku Salumu Mbonde akihusishwa na kujiunga na klabu ya Simba.Paul Ngelema na Juma Mpakala nao wanatajwa kuikacha klabu hiyo.

Pamoja na hayo yote kuendelea kwenye klabu hiyo, Uongozi kupitia kwa Ofisa Habari, Thobias Kifaru, umeendelea kudai kuwa kila kitu kipo sawa na hakuna matatizo yoyote kwenye klabu hiyo.

Comments