Moyes azua kizaazaa baa

Kocha aliyefukuzwa kazi Manchester United, David Moyes anasemekana amesababisha valangati kwenye baa moja iliyopo Clitheroe, Lancashire.

Moyes anadaiwa kumpiga kijana mwenye umri wa miaka 23 kwenye baa iitwayo Emporium hiyo maarufu kwa kuuza mvinyo.

Polisi wameanza uchunguzi juu ya tuhuma hizo za jinai, kwa sababu waliitwa na kuarifiwa juu ya kuumizwa kwa kijana huyo.

Kasheshe hiyo ilitokea Jumatano hii mwendo wa saa nne usiku na inaelezwa kwamba Moyes hakumpiga kijana huyo kiasi cha kwenda hospitali, lakini alikuwa akigugumia kwa maumivu.

Moyes anahojiwa lakini hajatiwa ndani, ambapo pamekuwa na maelezo ya kutofautiana juu ya kilichotokea hasa kwenye ulevi huo.

Moyes alifukuzwa kazi mwezi huu baada ya kuhudumu Manchester United kwa miezi 10 tu akichukua nafasi ya Sir Alex Ferguson.

Kabla ya hapo Moyes alikuwa kocha wa Everton alikodumu kwa miaka 11. Alishindwa kabisa kuwaongoza United, kwani waliishia nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, chini hata ya Everton na Tottenham Hotspur na hivyo kukosa ushiriki wa mashindano ya Ulaya.

Haijajulikana kwa hakika iwapo kijana huyo alimkejeli Moyes kwa kushindwa kazi aliyosomea au ilitokana na kilevi kuzidi kichwani mwa mmoja wao. Bado Moyes hajapata timu ya kufundisha.

Comments