Wane tu wana uhakika Man United

*Van Gaal aapa kutembeza panga

Kocha mpya wa Manchester United, Louis van Gaal amepanga kutembeza panga klabuni hapo na anaona ni wachezaji wane tu hadi sasa wanaweza kuwa na uhakika wa kubaki kikosini.

Van Gaal atakayeanza kazi baada ya kumaliza mkataba wake na Uholanzi kwenye michuano ya Kombe la Dunia, anachukua nafasi ya David Moyes aliyehudumu kwa miezi 10 tu na kushindwa kazi aliyoacha Sir Alex Ferguson.

Kocha huyo ambaye ni mkali kwa wachezaji na hana utani kwenye suala la nidhamu, amefanya tathmini ya wachezaji waliopo na anaona utata mtupu kwa sababu hakuna wenye kiwango anachokitaka isipokuwa wane tu.

Wachezaji waliohakikishiwa kubaki ni raia mwenzake wa Uholanzi, Robin van Persie, golikipa David de Gea, Wayne Rooney na Juan Mata, hivyo wengine wanaweza sasa kuanza kutafuta timu.

Old Trafford iliyokuwa ngome ya kutisha iligeuka uchochoro mbele ya hata timu dhaifu kwenye msimu uliopita na sasa hawamo kwenye mashindano yoyote makubwa ya Ulaya, kwani walimaliza katika nafasi ya saba.

Van Gaal (62) aliyefundisha timu kubwa kama Ajax, FC Barcelona na Bayern Munich kwa mafanikio, anataka kuona jinsi wachezaji wengine watakavyojibadili, pengine kwa kwenye Kombe la Dunia, vinginevyo baada ya usajili watakaobaki watasugua benchi.
 

Comments