Rais wa Bolivia asajiliwa kucheza soka

Wakati klabu zikijipanga kufanya usajili wa nguvu, Rais wa Serikali ya Nchi ya Bolivia, Evo Morales naye amesajiliwa kucheza soka ya kulipwa.
Morales, mwanasoka wa siku nyingi amekubali kusajiliwa na klabu ya Sports Boys ya nchini mwake kwa ajili ya msimu ujao wa soka.

Morales amesajiliwa na klabu hiyo yenye makazi yake katika Jimbo la Kusini Mashariki mwa nchi la Santa Cruz.

Klabu hiyo imesema kwamba Rais Morales atakuwa akicheza walau dakika 20 kwenye mechi, kutokana na kazi zake nyingi za kuongoza nchi.
Morales (54) atakuwa akilipwa kima cha chini cha mshahara cha pauni 127 na klabu hiyo ya daraja la kwanza.

“Anapenda soka na pia anaweza kucheza vizuri, atavaa jezi namba 10. Tutamtumia orodha ya mechi zetu na yeye atachagua zile ambazo atapata nafasi,” akasema Rais wa Klabu ya Sport Boys, Mario Cronenbold.

Mwanasiasa wa Jimbo la Santa Cruz aliye katika chama tawala cha Movement towards Socialism (MAS), Edwin Tupa amesema hatimaye ndoto ya Rais Mirales kucheza soka ya kulipwa imekamilika.

Inaelezwa kwamba rais huyo ni mtu wa mazoezi na yupo fiti kucheza na anasubiri kwa hamu msimu uanze. Amekuwa akicheza soka ya ridhaa katika mechi zinazotangazwa sana na waandishi wa habari, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na viongozi wengine.

Mwaka 2007 alicheza mechi kwenye uwanja uliokuwa futi mita 6,000 juu ya usawa wa bahari katika jitihada za kuwakosoa waliokuwa wakipinga nchi hiyo kupanga mechi zake kuchezwa uwanda wa juu sana kutoka usawa wa bahari.

Mwaka mmoja kabla ya hapo alivunjika pua baada ya kukabiliana na kipa akiwa dimbani.

Comments