Safari ya Taifa Stars kuanza kesho…

SAFARI ya timu ya soka Taifa ya Tanzania( Taifa Stars) kuanza kampeni ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa Afrika ( AFCON) inatarajia kuanza kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa kuikaribisha Zimbabwe.
Mechi hiyo ya kwanza itaanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij, amesema kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu na yenye ushindani kwa pande zote mbili.
Nooij alisema kwamba Taifa Stars wamejipanga vyema kupambana ili kusaka ushindi kwenye uwanja wa nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Alisema kwamba kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na maandalizi waliyofanya yatawaweka katika nafasi nzuri kuanza vyema kampeni za kuelekea Morocco.
” Ni mechi ngumu na yenye changamoto za kila aina…vijana wako imara na tayari kusaka ushindi”, alisema Mholanzi huyo.
Alieleza kwamba wachezaji wake wako vizuri na hana majeruhi kwenye kikosi hiko kilichokuwa kimeweka kambi jijini Mbeya na kurejea Dar es Salaam Jumanne.
Naye nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘ Cannavaro’ alisema kuwa watapigana kufa na kupona ili kuhakikisha wanashinda.
” Mechi hizi mbili ni za mtoano hivyo tutahakikisha tunashinda hata kama ni kwa goli moja, tukilipata tutalilinda huko ugenini”, alisema Cannavaro.
Kocha msaidizi wa Zimbabwe, Kalisto Pasuwa, alisema kuwa mechi hiyo ni ngumu na wachezaji wao wanafahamu wamekuja Tanzania kupambana.
Pasuwa alisema wanaamini wataanza vyema mashindano hayo na kupata nafasi ya kusonga mbele.
Taifa Stars na Zimbabwe zitarudiana baada ya wiki mbili na mshindi atakutana na Msumbiji au Sudan Kusini.
Hiyo ndiyo mechi ya kwanza ya mashindano kwa Nooij aliyerithi mikoba ya Mdenmark,Kim Poulsen.

Comments