Hakuna kulala Ligi Kuu Tanzania

Ligi Kuu ya Tanzania iliyomalizika hivi karibuni ilipelekea kushuka daraja kwa timu tatu ambazo ni Rhino Rangers ya Tabora, JKT Oljoro ya Arusha na Wauza Mitumba wa Ilala, Ashanti United.

Wakati hayo yakitokea, Ligi Daraja la Kwanza pia ilimalizika kwa timu za Stand United kutoka mkoani Shinyanga, Polisi Morogoro ya Morogoro na Ndanda FC ya Mtwara kufanikiwa kupanda daraja na watashiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Ndanda FC walio chini ya Kocha Mkuu Dennie Kitambi, wanatarajia kutumia Sh milioni 30 katika usajili ili kujiimarisha.
Huko ni katika kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu wa kocha huyo, timu ya Ndanda itahitaji wachezaji wanane wapya kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye sehemu ya beki, kiungo na safu ya ushambuliaji.
Kwa upande wa Stand United, Kocha Fulgence Novatus anasema timu yake imeamua kuitumia michuano ya mabingwa wa mikoa inayoendelea kwa sasa kwenye mikoa mitatu hapa nchini kama sehemu ya kung’amua vipaji ili kupata wa kuongeza kwenye kikosi chake.

Kwa sasa kocha huyo yuko mkoani Morogoro akifuatilia michuano hiyo na falsafa yake ni kuhakikisha anasajili wachezaji wenye umri mdogo na vipaji vya hali ya juu.
Timu ya JKT Oljoro baada ya kushuka daraja hawajakata tamaa na sasa wamejipanga kuja upya.

Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa, inatarajia kuingia kambini Mei 25 mwaka huu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Wanawahakikishia wadau wa michezo kwamba wanarudi tena Ligi Kuu. Oljoro walijikuta wanamaliza kwenye nafasi ya 13 kati ya timu shiriki 14 baada ya kujikusanyia alama 19 tu kutokana na michezo 26 waliyoshiriki.

Katika hatua nyingine, timu hiyo imeanza mikakati ya kuanzisha timu mbalimbali za michezo tofauti na soka.

Oljoro wanajiandaa kuanzisha timu nyingine zikiwamo za ngumi, riadha na mpira wa wavu. Hii ni habari njema kwa wadau wa michezo Tanzania. Hiyo ni kwa sababu michezo hiyo itaibua vipaji lukuki ambavyo kwa siku za usoni wachezaji watakuja kuwa sehemu ya wanamichezo watakaopeperusha bendera yetu ya taifa kwenye anga za kitaifa na kimataifa.

Comments